oksijeni

Kiungo cha pili kwa wingi katika mchanganyiko wa gesi unaounda angahewa. Hushika asilimia 20.95 ya ujazo wake, ukiwepo hewani zaidi katika umbo lake la diatomiki (O2). Molekuli za oksijeni hupasuka (dissociate) zaidi katika angahewa la juu, na kuzalisha atomi huru za kiungo hicho. Kama nitrojeni, ni gesi isiyo na rangi, isiyo na harufu, na isiyo na ladha, muhimu kwa uhai, ambayo viumbe hai huitumia kupitia upumuaji. Shughuli ya usanisinuru (photosynthesis) ya mimea na viumbe wengine kama vile sayanobaktiria (cyanobacteria) na fitoplanktoni ya baharini ndicho kichocheo kinachohusika na kuijaza tena, kuiongeza hewani.