lidar

Chombo au mbinu inayotumia teknolojia ya leza (laser) katika Hali ya Hewa. Neno hili ni kifupi cha Laser Imaging Detection And Ranging (LIDAR). Kwa kutoa mipigo ya miale ya leza, chombo cha lidar kina uwezo wa kubaini umbali hadi kwenye kitu au uso fulani, kutokana na kupima muda unaopita kati ya utoaji wa mpigo huo na kugundulika kwa ishara iliyorudishwa (rejeshi). Miongoni mwa matumizi ya kihali ya hewa ya vyombo hivi ni, kwa mfano, kupima kimo cha dari ya mawingu katika viwanja vya ndege (ceilometa), kubainisha sifa za erosoli katika safu za angahewa, na kupima upepo wa tabaka za juu za anga.